Tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Maweni kijijini hapo wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Mbeya. Msaidizi wa zamani wa Padri (Katekisita) katika
Kigango cha Kanisa Katoliki Kijiji cha Mkwajuni, Florian Mwamosi (70) amekufa
baada ya kuzikwa akiwa hai katika kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua kwa njia
ya kishirikina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani alikiri kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa lilitokea saa 9:00 mchana katika kijiji hicho cha
Maweni Mkwajuni wilayani Chunya.
“Marehemu aliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa
na mawe kwa tuhuma za kuhusika na uchawi na kusababisha kifo cha Peter Robert,”
alisema.
Kamanda Athumani alisema kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio
hilo unaendelea na kwamba wahusika wote wa tukio hilo wamekimbia na kuzihama
nyumba zao, hivyo polisi wanaendelea na msako wa kuwatia mbaroni watuhumiwa na
kwamba tayari kaburi hilo limefukuliwa
jana kutenganisha maiti hizo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa marehemu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kwa
ushirikina aliwahi kuwa Katekista wa kigango hicho hadi mwaka 2007.
Wameeleza kuwa Mwamosi alikwenda kuhudhuria mazishi ya
Peter Robert (28) katika kitongoji hicho
cha Maweni, baada ya kufuatwa nyumbani kwake na watu wakitaka aende kwa sababu
yeye ni mmoja wa wazee wa mila katika kitongoji hicho.
“Bwana Mwamosi alikuwa akituhumiwa kwa uchawi kwa muda mrefu
na wenzie wawili, hivyo alipofika makaburini ilianza minong`ono ya watu na huku
wengine wakiguna na ndipo alipoombwa aingie kaburini kwa ajili ya kupokea
jeneza lililobeba mwili wa marehemu Peter Robert,” alisema mkazi mmoja wa
kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph.
Alisema kuwa baada ya kuingia kaburini akiwa na watu wengine
watatu wenzake walitoka kwa haraka na kumwacha Mwamosi peke yake ndipo kundi la
watu waliokuwa eneo hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe
huku wakimwamuru akae chini.
Shuhuda huyo alisema kuwa baada ya kukubali kukaa chini
akiwa ndani ya kaburi hilo, walianza kumfukia na alipofukiwa nusu ya mwili wake
waliingiza jeneza la marehemu Peter na kuliweka juu yake na kuanza kulifukia
kaburi hilo.
“Baada ya kukaa chini ndani ya kaburi hilo ndipo walianza
kumfukia kwa udongo na baadaye wakachukua jeneza la marehemu na kuliweka juu
yake, kisha kumfukia na udongo na taratibu za mazishi ziliendelea kwa ajili ya
marehemu Peter,”alisema.
Alidokeza kuwa chanzo cha tukio hilo ni marehemu Robert
kuugua ghafla tumbo, ndipo ndugu zake walipoamua kumpeleka kwa mganga wa jadi
kwa ajili ya kupata matibabu na baada ya siku tatu alifariki dunia.