Fedha hizo ni zile zilizolalamikiwa na wabunge wakati wa
uwasilishwaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika pamoja na ile ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Kutokana na kuwapo mvutano mkali bungeni, kwa nyakati
tofauti Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, walilazimika kutoa maelezo ya
kina kuwashawishi wabunge wakubali ili fedha hizo ziidhinishwe katika bajeti
husika kwa ajili ya matumizi ya mwaka mpya wa fedha unaoanza Juni mwaka huu.
Fedha hizo ni Sh74 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mfuko
wa pembejeo, Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa kitaifa, Sh88
bilioni za Ruzuku ya Mfuko wa Pembejeo na Sh29 bilioni kwa ajili ya kufuatilia
utekelezwaji wa miradi ya Serikali.
Baadhi ya wabunge walilalamikia fedha hizo wakisema kuwa ni
ulaji kwa wakubwa.
Wakizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT),
Profesa Tolly Mbwete alisema kwa kuwa Bajeti ya Wizara ya Fedha itapitishwa
mwishoni, wabunge wanatakiwa kuikataa hadi mambo muhimu katika bajeti
zilizotangulia kusomwa, yatakapofanyiwa kazi.
“Binafsi naona hiyo ndiyo njia nzuri iliyobaki, wabunge
wanatakiwa kuamua mambo kwa masilahi ya taifa na siyo kwa manufaa na maslahi
yao binafsi,” alisema Profesa Mbwete.
Aliwataka wabunge kutumia fursa hiyo kumbana Waziri wa Fedha
ili kuhakikisha kuwa fedha zaidi zinaongezwa, au kupunguzwa katika maeneo
mengine, kwa ajili ya kupelekwa katika maendeleo.
Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),
alisema kuwa fedha zaidi zinatakiwa kuongezwa katika bajeti ya maendeleo,
badala ya matumizi ya kawaida.
Aliongeza pia kwa kusema“Maendeleo yatapatikana kwa haraka kama tutawekeza zaidi ya
asilimia 20 ya bajeti yetu kwenye matumizi ya maendeleo. Hii ni tofauti na
sasa, ambapo asilimia 90 ya fedha zinazotengwa zinakwenda katika matumizi ya
kawaida,” .