9.12.12

GARI LA MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA SUA LIMETEKWA NA KUAHARIBIWA VIBAYA NA KUWAJERUHI WASINDIKIZAJI NA KUWAPORA KILA KITU




Pichani ni mmoja wa Mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Mkoa  Singida, akijaribe kurekebisha mapambo ya jeneza lililokiwa na mwili wa marehemu Munchari Lyoba,baada ya kuharibiwa

Majambazi, wamevamia gari lililokuwa linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha kupora fedha pamoja na vitu mbalimbali vyenye dhamani ya  takriban Shilingi milioni 19 za kitanzania,Ni fedha na vitu walivyokuwanavyo waombolezaji.
 Tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi mkoani Singida,  majambazi hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na jeneza lililokuwa na mwili wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi  wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na kumpekua marehemu.
JANA akizungumza na waandishi wa habari nje ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa msafara uliokuwa ukisafirisha maiti, Makaranga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 usiku katika gari aina ya Land Cruiser mali ya SUA.
WAKATI akisimulia tukio hilo, Makaranga alisema kuwa lilitokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa Singida kwenye kona maarufu kwa jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani Mara.  
Alisimulia kwamba gari hilo pamoja na jeneza, lililobeba viongozi wa wanafunzi sita na viongozi wengine wanne lilipofika eneo la tukio, walikuta mawe makubwa yamepangwa barabarani na kuwalazimisha kusimama ndipo wakavamiwa na kundi kubwa la vijana, ambao walibeba bunduki mbili aina ya gobore, marungu, mashoka na mawe.  
“Walipofika walipiga kioo cha gari letu kwa mbele na kumparaza kwa panga usoni dereva wetu. 


Baada ya hapo walivunja vioo vyote na kutuamuru kutoa kila kitu tulichokuwa nacho,” Makaranga akisimulia.  
Pia Makaranga aliongeza kwa kusema, kuwa katika tukio hilo, aliporwa Sh2 milioni alizokabidhiwa azihifadhi kwa ajili ya kugharimia msafara huo, Sh8.8 milioni zilizochangwa na wanafunzi kama rambirambi kwa  mwenzao na jumla ya Sh9 milioni ambazo wasindikizaji walikuwa nazo mifukoni mwao.  
“Pia tuliporwa simu  zetu zote  za mikononi, viatu, laptop na mabegi yote ya nguo zetu,” alisema.  
Makaranga aliyeeleza kuwa anafanya kazi za kiutawala SUA, aliwataja walioumizwa na majambazi hao kuwa ni pamoja na yeye, dereva wao na kiongozi wa wanafunzi, Idd Idd ambao walitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kuruhusiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa amewasiliana na uongozi wa SUA ili watume gari lingine na kukarabati jeneza lililoharibiwa na majambazi hao.
Mlozi aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Kamati ya Ulinzi na Usalama, watahakikisha watu waliofanya unyama huo, wanakamatwa haraka iwezekanavyo ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.  


“Tukio hili limenisikitisha sana, maana sasa binadamu wametokwa na utu wa ubinadam kwenye akili zao na kuhamia kwenye vitendo ambavyo si vyakiungwana kabisa na kamwe hawezi kuthubutu kuvifanya mtu mwenye akili timamu na utu, maana watu wanapekua hadi maiti na kuisachi!".